Latest News

Tuesday, 29 March 2016

Chad kumvunja moyo Mkwasa





Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars Charles Mkwasa amesema kitendo cha Chad kujitoa kwenye michuano ya Afrika kimemnyong’onyesha. Chad iliyokuwa icheze mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2017 dhidi ya Stars jana, ilitangaza kujitoa kutokana na ukata.

Akizungumza jana, Mkwasa alisema timu yake ilishajiandaa kushinda mechi ya jana na kwamba wachezaji walikuwa kwenye ari kubwa. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini N’Djamena Jumatano iliyopita, Stars ilishinda bao 1-0 na kufufua matumaini kwenye michuano hiyo.

“Baada ya ushindi ule wachezaji wangu walikuwa kwenye ari kubwa na walikuwa na uhakika wa kushinda mechi ya marudiano, lakini jambo la kujitoa kwa wapinzani wetu limetunyong’onyesha wote,” alisema.
Aidha Mkwasa alilaumu kwamba vitendo kama jivyo ndivyo vinavyosababisha soka ya Afrika haipigi hatua kwa baadhi ya nchi kutokana na kutokuwa makini. “Soka ya Afrika kwa baadhi ya nchi haiwezi kwenda mbele zaidi, hili linakatisha sana tamaa hatuna tu la kufanya,” alisema.


Kitendo cha Chad kujitoa kimefanya matokeo yake yote ya mechi ilizocheza kufutwa na hivyo Misri kubaki ikiongoza kundi hilo kwa pointi 4 ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi 2 na Tanzania inashika mkia ikiwa na pointi moja. Nigeria na Misri zinatarajiwa kucheza leo.

Hata hivyo Mkwasa alisema hawatakata tamaa kupambana mpaka dakika ya mwisho katika mechi zilizosalia licha ya kufahamu kwamba wapo kwenye mazingira zaidi kwa sasa. Stars inatarajiwa kucheza na Misri Juni 4 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, mechi ya kwanza iliyofanyika Cairo Stars ilifungwa mabao 3-0 na kuwa na kazi nguvu ya kubadili matokeo.

Fainali za michuano hiyo zitafanyika Gabon, na Stars itamaliza mechi zake za kufuzu ugenini dhidi ya Nigeria Septemba mwaka huu. Mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.


No comments:

Post a Comment